MAKUMBUSHO YA TAIFA YAJITOSA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MIMBA ZA UTOTONI

Imewekwa: 28th August, 2018

Makumbusho ya Taifa yajitosa Mapambano ya Mimba za Utotoni

Na Joyce Mkinga

SIKUJUA (siyo jina lake halisi) msichana wa miaka kumi na tatu amelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana akiwa na hali mbaya akisubiria kufanyiwa upasuaji baada ya kupata ujauzito akiwa darasa la sita na mwanaume aliyempa ujauzito huo hajamtia machoni tangu afanye naye tendo la ndoa na kumpatia sh 10,000/-.

Afya ya Sikujua imedhoofu sana, wazazi wake hawana uwezo mkubwa wa kumsaidia kimatibabu kwa sababu ujauzito huo umekuwa wa shida na karaha nyingi kutokana na kuumwa mara kwa mara.

Kweli majuto ni mjuu!, Najuta kumjua Hamisi, mwanaume aliyenipa mimba hii! Hatma ya maisha yangu haijafahamika bado, nahisi nitakufa na mimba hii, alinidanganya kuwa kwakuwa nafanya tendo hilo kwa mara ya kwanza eti sintopata mimba, kumbe kanidanganya” anasema Sikujua kwa kilio cha uchungu mkubwa.

Sikujua ni mmoja tu kati ya watoto wa kike wengi wanaokumbwa na maswaiba ya kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo. Wengi wao hupata madhara makubwa ya kiafya ikiwepo fistula na wengine kupoteza maisha yao kabisa.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani ( UNICEF ) mwaka 2017, Tanzania ni nchi ya tatu kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na viwango vya juu vya mimba na ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Kwa nchi ya Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 28. Nchini Kenya, ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ni ukiukaji wa haki za kibinadamu. Hii ni kwa sababu mimba za utotoni ni moja ya sababu zinanazomnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu.

Ripoti hiyo ya UNICEF imeeleza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watoto na wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walimu, na wadau wengine juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni.


Kwa kulitambua hili Makumbusho ya Taifa hapa nchini kwa kushirikiana na wadau wengine inatekeleza Mradi wa Mapambano Dhidi ya Mimba za Utotoni kwa njia ya Sanaa kupitia mradi wao maarufu ujulikanao kama Museum Art Explosion Against Adolescence Pregnancy.

Lengo kuu la mradi huu wenye Kaulimbiu ya Mtoto wa Kike Washa Taa ni kutoa elimu kwa watoto walio chini ya miaka 18 hususani wanafunzi wa shule za msingi na sekondari juu ya kupambana na mimba za utotoni kwa kutumia sanaa mbalimbali zikiwemo za jukwaani na za ufindi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw Achiles Bufure anasema mradi huu una lenga katika kutoa elimu kwa watoto, wazazi na wadau wengine juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni.

Watoto wamekuwa wakijihusisha na ngono zembe kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa uelewa, mila potofu na vishawishi mbalimbali, na hili la uwelewa si kwa watoto tu bali hata kwa watu wazima ambao ndio wamekuwa chanzo kikubwa cha changamoto hii ndio maana tumeamua kuja na program hii ili tuweze kupambana na hili janga.” anasema Bw. Bufure.

Mradi umeendesha mafunzo kwa wasanii, wanafunzi, walimu na wadau mbalimbali juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni katika ngazi za familia hadi taifa ili kwa pamoja kuwe na nguvu moja ya kupambana na changamoto hiyo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Nuru Kitara, Afisa Maendeleo ya jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anasema tatizo la mimba za utotoni ni changamoto kubwa katika nchi yetu kwa sababu watoto wa kike wamekuwa wakipata ujauzito au kuolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Anataja mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni kuwa ni Shinyanga kwa asilimia 59, Mara kwa asilimia 55, Dodoma asilimia 51 na Lindi asilimia 48. Mingine ni, Mbeya kwa asilimia 45, Morogoro na Singida asilimia 42, Rukwa asilimia 40 na Ruvuma asilimia 39.


Dkt. Kitara ameongeza kuwa Wasichana wa vijijini wana uwezekano wa karibu mara mbili ya wale wa mijini wa kupata watoto kabla hawajafikia umri wa miaka 19 na pia nusu ya wasichana ambao hawakupata elimu hupata watoto au mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 19, ikilinganishwa na kama asilimia 25 kwa wasichana waliomaliza elimu ya msingi.


Watoto waliozaliwa na mama wa umri mdogo wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kuliko wale waliozaliwa na mama wa umri mkubwa, visababisho vya mimba za utotoni na kuolewa mapema ni pamoja na Mila na desturi zenye madhara, uelewa mdogo wa watoto wa kike kuhusu muda na vipindi wanavyoweza kupata ujauzito na wazazi kutokutimiza majukumu yao ya malezi kwa watoto kikamilifu”. Alisema Dkt Ktara

Dkt. Kitara aliendelea kutaja sababu zingine kuwa ni baadhi ya wasichana hulazimishwa kuolewa au hukataliwa na familia zao jambo ambalo huwaweka katika hatari zaidi ya kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na matatizo ya kiuchumi yanaweza kusababisha wasichana wadogo kujihusisha na biashara ya ngono.

“Tunahitaji kutoa elimu kwa watoto na wazazi juu ya madhara ya mimba za utotoni ili kuwaokoa watoto na jamga hili,” anasema Dkt. Kitara.

Dkt. Kitara anasema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kupamba na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kusaini na kuridhia Mikataba mbalimbali inayohusu haki za Mtoto, kuandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto na kutungwa kwa Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009. Vile vile Serikali imekuwa ikiendesha kampeni ya Mimi Msichana najitambua Elimu ndiyo mpango mzima iliyozinduliwa Octoba, 2017.


Tunahitaji kutoa elimu kwa watoto na wazazi juu ya madhara ya mimba za utotoni ili kuwaokoa watoto na jamga hili hivyo nitoe wito kwa wadau mbalimbali kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya mimba za utotoni ili kujenga Tanzania yenye maadili mema” Aliongezea Dkt. Kitara.


Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimeboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma nzuri za afya kwa vijana katika wilaya husika, kusimamia shule zote zifundishe stadi za maisha kwa shirikiana na vyama vya kiraia, kufuatilia mwenendo wa mahudhurio na ukatishaji wa masomo shuleni na kuhimiza shule zote zitilie mkazo katika kuhakikisha mahudhurio mazuri na wanafunzi wanasoma mpaka wahitimu.


Naye Amabilisi Batamula kutoka FEMINA anasema kuna haja ya kuwa na mkakati wa uhamasishaji na uelimishaji jamii wenye tija juu ya madhara ya mimba za utotoni, watoto bila kujali kuwa ni msichana au mvulana, aelewa matokeo ya mimba zisizotakiwa, wajifunze namna ya kuzuia mimba zisizotakiwa na waeleweshe marafiki zako pia wawatambua wasichana wanaopata ujauzito na kuwashawishi waendelee na masomo.

Sanaa iwe ya jukwaani au ya maonesho ina mchango mkubwa katika kutoa elimu kwa wadau hivyo ni vyema wa sanii mliopata fursa hii, itumieni vyema katika kutoa mchango wenu kwa jamii juu ya mapambano haya ya mimba za utotoni maana Sanaa ni njia muafaka ya kufikisha ujumbe kwa jamii kwa haraka zaidi” anasema Bibi Batamula.

Mratibu wa Mradi wa Museum Art Explosion Against Adolesence Pregnancy, Edger Joel anasema katika mradi huu wa kutoa elimu kwa njia ya sanaa, aina zote za sanaa zitatumika ikiwa ni pamoja na sanaa za jukwaani na za ufundi ili kutoa nafasi kwa kila mwanajamii kujifunza kwa kupitia aina ya sanaa anayoipenda.

Anasema mwisho wa mwezi wa Septemba kutakuwa na onesho kubwa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni ambapo wanafunzi, walimu, wazazi na wadau mbalimbali watashiriki katika onesho hilo.

Mwishoni mwa mwezi Septemba, wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake watapata nafasi ya kuona maonesho makubwa ya sanaa kutoka kwa wasanii nguli hapa nchini, sanaa hizo ni pamoja na michoro, vinyago, ubunifu wa mavazi, maigizo, musiki, ngoma na majigambo mbali mbali kwenye kumbi zetu za kisasa zilizopo hapa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam,Posta”. Aslisema Bw Chatanda.

Bw Chatanda alimalizia kwa kusema kuwa baada ya maonesho ya jijini Dar es Salaam, maonesho hayo pia yanatarajiwa kufanyika katika Mikoa ya Shinyanga wilaya za Shinyanga vijijini, Kishapu na Kahama na Mkoa wa Tabora katika wilaya za Kaliua, Nzega na Igunga.

Mwisho