TANZANIA NDIO CHIMBUKO LA MWANADAMU DUNIANI

Imewekwa: 07th February, 2018

Na Sixmund J. Begashe

Watanzania wamehamasishwa kutembelea Makumbusho ya Taifa ili kujionea na kujifunza historia muhimu ya Chimbuko la Mwanadamu ambayo ni Tanzania pekee ndio imebarikiwa na utajiri wa urithi mkubwa wa historia hiyo.

Wito huo umetolewa na waziri wa Maliasili na Utalii nchini Dr. Hamisi Kigwagala kupitia hotuba iliyo somwa kwa niaba yake na Mkurugenzi mtendaji wa bodi ya Utalii nchini Bi. Devota Mdachi katika sherehe za ufunguzi wa Ukumbi wa Chimbuko la mwanadamu uliopoa Makumbusho ya Taifa, Posta Dar es Salam.

Bi Mdachi emeongeza kuwa onesho hili linaumuhimu mkubwa hasa kwa wanafunzi na watafiti mbali mbali kwakuwa litawapa nafasi ya kujifunza mengi juu ya uasilia wa Binadamu na pia kusaidia kuwaunganisha binadamu wote kwakuwa wote ni ndugu na asili yao ni Tanzania.

Nae Balozi wa Hispania hapa nchini, Mh. FELIX COSTALES amesema Onesho hilo lina umuhimu mkubwa kwa jiji la Dar es Salam na Tanzania kwa ujumla kwa kuwa watalii wengi watakuja Dar es Salaam kujionea Onesho hilo.

Akiwashukuru wageni na wananchi mbali mbali kwa kufika kwenye uzinduzi wa onesho hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa, Mama Anna Abdalah ameomba Bodi ya Utalii nchini kuhakikisha inawaelekeza watalii wote wanaoingia nchini kutembelea Makumbusho ya Taifa ili waweze kujifunza asili yao.

Nao wananchi mbali mbali waliohudhuria uzinduzi wa Onesho hilo wamesema kwao ni mara yao ya kwanza kushuhudia onesho kubwa la kihistori ya maisha ya mwanadamu ambalo vioneshwa vyote ni halisi na vimepatikana hapahapa Tanzania kitu kinachoendelea kuifanya Tanzania kuwa ya kipekee zaidi ya nchi zingine ulimwenguni.

Mimi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mlimani nasomea Menejimenti ya Urithi wetu, kwa kweli onesho hili limeniongezea ufahamu mpana zaidi ya ule nilioupata darasani, mimi nitoe wito kwa wanafunzi wote nchini na wale wasio wanafunzi kuja hapa Makumbusho ya Taifa kujionea wenyewe onesho hili muhimu kwa historia ya Dunia kwa ujumla, hakika watakao kuja watafurahi sana na kujifunza mengi kama hivi leo mimi hapa.” Alisema Abasi Ramadhani.

Onesho hilo lililohudhuriwa na Mabalozi mbalimbali wa nje hapa nchini na mamia ya wananchi kutoka sehemu mbali mbali, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof Audax Mabula kuwa limebeba sehemu nne muhimu ambazo ni Ushahidi wa Nyayo za Zamadamu aliyetembea kwa miguu miwili miaka milioni 3.6 iliyopita, ugunduzi wa zana za mawe, Jamii inayofanana na binadamu na sehemu ya Mwisho ni ya mwanzo wa binadamu wa sasa miaka laki 2 iliyopita.