emblem

The United Republic of Tanzania

The National Museum of Tanzania (NMT)

BG IMAGE

Welcome to National Museum

Service Category

News

Uwanja wa Taifa kuwa kivutio cha Utalii


Na Mwandishi Wetu,

Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa kushirikiana na uongozi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wameanza mikakati ya kufanya Uwanja wa Taifa kuwa kivutio cha utalii kupitia maonesho ya kihistoria ya uwanja huo.

Hayo yamedhihirika baada ya mkutano kati ya Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Yusuf Singo Omar na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dr Noel Lwoga.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, walijadili masuala mbalimbali ikiwemo la kuanzisha makumbusho ya michezo katika uwanja huo.

Viongozi hao pia walijadili kuhusu ushirikiano kwenye uhifadhi na kuendeleza malikale na urithi wa utamaduni wa Tanzania ikiwemo Uwanja wa Uhuru uliojengwa kabla ya Uhuru wa Tanzania (mwaka 1947).

Vile vile walijadili na kukubaliana juu ya kuandaa maonesho au kuanzisha Makumbusho ya Historia ya Michezo Tanzania ambayo yanaweza kuwekwa uwanjani hapo.

Mjadala wao pia ulijikita katika kutumia Uwanja wa Taifa katika kuitangaza Makumbusho ya Taifa na malikale lukuki zilizopo nchini.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na Kurugenzi ya Michezo katika kuvifanya viwanja vya Taifa kuwa vutivu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi na kuwa sehemu nzuri ya utalii.

“Tumezungumza vizuri na wenzetu na sisi kama watalaamu wa uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni tutahakikisha viwanja hivi vinavutia watalii kutembelea kabla na baada ya mechi zao,” alisema Dkt. Lwoga.

Amesema jiji la Dar es Salaam lina vivutio vingi vya asili ikiwemo makumbusho, majengo, fukwe, bustani na uwanja wa Taifa na kwamba inahitajika elimu kwa watu kujua viko wapi ili waweze kutembelea.

Naye Mkurugenzi wa Michezo, Bw Yusufu Omar amesema ushirikiano na Makumbusho ya Taifa ni wa muhimu katika kuendeleza malikale nchini ikiwemo Uwanja wa Taifa.

“Sisi kwa upande wetu tumefurahi sana maana ushirikiano huu umekuja wakati muafaka,” alisema Omari.

Amesema uanzishaji wa makumbusho katika Uwanja wa Taifa utasaidia kuleta watu wengi zaidi watakaopenda kuja kujifunza.

MWISHO