Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

MAKUMBUSHO YASHIRIKI KONGAMANO LA UTALII, UWEKEZAJI NA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MISRI

Imewekwa: 16 Jun, 2026
MAKUMBUSHO YASHIRIKI KONGAMANO LA UTALII, UWEKEZAJI NA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MISRI

Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeshiriki katika Kongamano la Utalii, Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Misri lililolenga kuhamasisha fursa za uwekezaji, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya mataifa hayo mawili.

Kongamano hilo lilileta pamoja wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya sekta ya utalii. Kwa upande wa Tanzania, shughuli za kongamano hilo ziliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.

Siku ya pili ya kongamano ilitengwa mahsusi kwa ajili ya masuala ya utalii, ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mikakati ya pamoja ya kukuza utalii na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Misri katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

Ushiriki wa Kimkakati kwa Maendeleo ya Utalii wa Urithi

Akizungumza kuhusu ushiriki wa NMT katika kongamano hilo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa Umma wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Bi. Pendo Gondwe, alisema kuwa ushiriki huo ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kukuza utalii wa utamaduni, urithi na malikale nchini.

Alieleza kuwa kupitia kongamano hilo, NMT imepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya urithi wa taifa vinavyohifadhiwa na kusimamiwa na taasisi hiyo, kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea makumbusho, maeneo ya urithi wa utamaduni na malikale nchini Tanzania.

Aidha, NMT imeweza kunadi fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya makumbusho, urithi na malikale, pamoja na kuvutia wabia wa maendeleo watakaosaidia kuboresha huduma, miundombinu na bidhaa za utalii wa urithi nchini.

Kupitia kongamano hilo, NMT pia imepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali wa sekta ya urithi na utalii kutoka Misri, nchi inayotambulika duniani kwa mafanikio makubwa katika usimamizi wa makumbusho, maeneo ya kihistoria na vivutio vya urithi wa dunia.

Vilevile, ushiriki huo umefungua fursa za kujifunza mbinu na teknolojia za kisasa za uhifadhi, tafsiri na uwasilishaji wa urithi wa kitamaduni kwa umma, pamoja na kuweka msingi wa ushirikiano wa baadaye kupitia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya taasisi za makumbusho za Tanzania na Misri.

Ushiriki wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kongamano hili unaakisi dhamira ya taasisi ya kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa urithi na utamaduni, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuifungua Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi, biashara, uwekezaji na utalii.

Jitihada hizi zinaendelea kuchangia kukuza uchumi wa taifa na kuongeza mchango wa sekta ya urithi wa utamaduni katika maendeleo endelevu ya Tanzania.

#TumerithishwaTuwarithishe