Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

ZIARA YA MAMA JANETH MAGUFULI YAIBUA UMUHIMU WA UHIFADHI NA KUTEMBELEA URITHI WA TAIFA

Imewekwa: 16 Sep, 2026
ZIARA YA MAMA JANETH MAGUFULI YAIBUA UMUHIMU WA UHIFADHI NA KUTEMBELEA URITHI WA TAIFA

DAR ES SALAAM, 15 SEPTEMBA 2026. Ziara ya Mama Janeth Magufuli katika Makumbusho ya Taifa la Tanzania jana imekuwa chachu ya kuhamasisha wananchi kutembelea Makumbusho na kujifunza historia, utamaduni na urithi wa Taifa la Tanzania.

Mama Janeth Magufuli, ambaye ni mke wa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametembelea maeneo mbalimbali ya Makumbusho ya Taifa na kujionea kwa karibu maonesho ya vitu na kumbukumbu mbalimbali za kihistoria zinazohifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika ziara hiyo, Mama Janeth amepata fursa ya kuona na kujifunza kuhusu baadhi ya vivutio na vitu vya urithi vinavyohifadhiwa na Makumbusho ya Taifa, ikiwa ni pamoja na ndege ya kihistoria aina ya Fokker F28 Fellowship yenye usajili 5H-CCM, ambayo ni miongoni mwa urithi unaobeba kumbukumbu muhimu za historia ya uongozi na maendeleo ya Tanzania.

Ziara hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa kuhifadhi, kutunza na kuthamini urithi wa Taifa, kwa kuwa vitu vya kihistoria na kumbukumbu zinazohifadhiwa katika Makumbusho ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa na chanzo cha elimu kwa vizazi mbalimbali.

Aidha, ziara hiyo inatoa wito kwa wananchi, hususan familia, vijana na wanafunzi, kutumia fursa zilizopo kutembelea Makumbusho ya Taifa ili kujifunza historia ya Tanzania, kufahamu utamaduni wa jamii mbalimbali na kutambua thamani ya urithi wa Taifa.

Makumbusho ya Taifa yanaendelea kuwakaribisha wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea maeneo yake mbalimbali, kujifunza na kushiriki katika juhudi za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

#TumerithisishwaTuwarithishe#