Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

“MATAMASHA YA UTAMADUNI NI CHACHU YA UTALII NCHINI” - DKT. CHANA

Imewekwa: 11 Oct, 2024
“MATAMASHA YA UTAMADUNI NI CHACHU YA UTALII NCHINI” - DKT. CHANA

Na Happiness Shayo - Dar es salaam 

Jamii nchini zimeshauriwa kufanya matamasha ya tamaduni zao katika Kijiji cha Makumbusho na katika maeneo yao ya asili ikiwa ni njia mojawapo ya kutunza na kurithisha Utamaduni kutoka kizazi hadi kizazi hali itakayovutia pia watalii wengi wa kiutamaduni nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt, Pindi Chana (Mb), alipozindua rasmi Tamasha la Utamaduni wa watu wa Kigoma Jijini Dar es Salaam, huku akiipongeza jamii hiyo kwa Tamasha hilo.

Waziri Chana amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kushirikiana na jamii katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni ikiwemo ujenzi na ukarabati wa nyumba za asili za Kijiji cha Makumbusho.

“Ni dhahiri kwamba kwa mashirikiano haya ya Serikali na wanajamii ya Mkoa wa Kigoma katika Tamasha hili hapa Kijiji cha Makumbusho, ni kielelezo cha jinsi ambavyo Serikali inatekeleza siyo tu sera za Taifa, bali pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi zake inazozitoa kwa wananchi” alisema Mhe. Chana.

Aidha, Mhe. Chana amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo na kulitumia kama fursa ya majadiliano ya kimaendeleo na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwahimiza Wananchi kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa pamoja na kujikwamua katika hali ya umaskini, ujinga na maradhi.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Makumbusho ya Taifa, Dkt. Oswald Masebo amesema kuwa Tamasha hilo la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania ni la Thelathini (30) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, na ni takribani makabila zaidi ya thelathini na saba (37) ambayo yamefanya maonesho yao tangu kuanzishwa utaratibu huo, kati ya makabila zaidi ya 120 yaliyopo nchini. 

Tamasha hilo kubwa ambalo limehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula  lililopambwa na Ngoma za asili, nyumba za asili, vyakula na vinywaji vya asili, mavazi ya asili, linatarajiwa kufungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip  Isdor Mpango tarehe 13 Oktoba 2024.