Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makumbusho ya Taifa la Tanzania

MAKUMBUSHO YA TAIFA YAWEKA MIKAKATI YA KUFUNGUA UKURASA MPYA WA UTALII WA MALIKALE PANGANI

Imewekwa: 18 Sep, 2026
MAKUMBUSHO YA TAIFA YAWEKA MIKAKATI YA KUFUNGUA UKURASA MPYA WA UTALII WA MALIKALE PANGANI

Pangani, Tanga – Septemba 17, 2026: Wilaya ya Pangani imeendelea kujidhihirisha kuwa eneo lenye utajiri mkubwa wa historia, utamaduni na urithi wa asili, huku jitihada za kuibua, kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza rasilimali hizo zikipewa msukumo mpya.

Hayo yamebainishwa katika kikao maalumu kilichofanyika Pangani kwa lengo la kutambua, kuainisha na kuweka mikakati ya pamoja ya kuendeleza na kutangaza maeneo mbalimbali ya utalii wa malikale yaliyopo wilayani humo.

Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Pangani, Bi. Ester Gama, akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga; Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malikale kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Emmanuel Bwasiri; pamoja na Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Gwakisa Kamatula.

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kuibua na kuendeleza rasilimali za kihistoria, kiutamaduni na kiasili zilizopo Pangani, ili kuzifanya kuwa sehemu muhimu ya shughuli za utalii na maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Juhudi hizo pia zinalenga kuongeza mwonekano wa Pangani katika ramani ya utalii wa Tanzania, kutokana na kuwa na urithi wa kihistoria na kiutamaduni pamoja na mandhari ya asili yenye uwezo wa kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Mji wa Pangani una historia pana inayohusisha urithi wa kihistoria na kiutamaduni, ambao ukiendelezwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi endelevu unaweza kutoa fursa zaidi za elimu, utalii, ajira na shughuli za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Makumbusho ya Taifa ya Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha maeneo ya urithi wa taifa yanaibuliwa, kuhifadhiwa na kutangazwa kwa ufanisi, sambamba na kuongeza fursa za wananchi kunufaika na rasilimali za urithi kupitia utalii, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

Kwa kuimarisha juhudi za pamoja katika uhifadhi, uendelezaji na utangazaji wa vivutio vya malikale, Pangani ina fursa ya kufungua ukurasa mpya wa utalii wa malikale na kuongeza mchango wa urithi wa taifa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.